Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Jeshi la Polisi Tanzania, URA SACCOS kimekabidhi Vifaa Tiba pamoja na Kompyuta kwa Vikosi vya Jeshi la Polisi Tanzania tarehe 22.08.2022.
Vifaa Tiba ni kwa ajili ya Zahanati ya Jeshi iliyopo Kunduchi Dar es salaam na Zahanati ya Jeshi la Polisi mkoa wa Simiyu. Kumpyuta kumi na mbili(12) zilizotolewa ni kwa ajili ya Vyuo vya Ufundi Stadi vilivyopo katika Kikosi cha Polisi Ujenzi na Bohari Kuu ya Jeshi la Polisi.
Akikabidhi katika hafla fupi iliyofanyika katika ofisi za URA SACCOS Makao Makuu jijini Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya URA SACCOS, Festo Christopher Ngwenuki amesema vifaa vyote hivyo vina thamani ya Tsh. 40,361,000 ikiwa ni kutimiza takwa la kisheria la kurudisha faida kwa jamii inayowazunguka.
Amesema Bodi ya Chama hicho pamoja na wanachama wanaamini Vifaa hivyo vitatumika kwa manufaa ya Jeshi la Polisi na wananchi kwa ujumla.
Awali, Mkuu wa Kikosi cha Afya, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Hussen Yahaya na Mkuu wa Kikosi cha Ujenzi Kamishna Msaidizi Fadhili Ishekazoba pamoja na Mboharia Mkuu Kamishna Msaidizi Moses Mziray kwa pamoja wamekishukuru Chama hicho kwa msaada huo kwani umekuja wakati muafaka. Hata hivyo wamesema Kompyuta zilizotolewa katika Vyuo hivyo vitawasaidia vijana wa Kitanzania katika kuwapa ujuzi utakaowapelekea kuweza kujiajiri na kuondokana na kujiunga na makundi mabaya ya mtaani. Vile vile Vifaa Tiba vitasaidia kuwatibu askari, familia zao pamoja na wananchi waishio jirani na Zahanati hizo.